YANGA iliyokuwa na mwanzo mbaya wa msimu,
hatimaye imeifikia Simba kileleni mwa msimamo wa Ligi Kuu ya Tanzania Bara
kufuatia ushindi wa 3-0 dhidi ya Mgambo JKT, huku Wekundu wa Msimbazi
waking'ang'aniwa kwa sare ya 1-1 dhidi ya timu ya mkiani ya Polisi kwenye Uwanja
wa Jamhuri mjini Morogoro jioni ya leo.
Ushindi
huo unamaanisha kwamba Yanga sasa imelingana pointi 23 na Simba kileleni baada
ya mechi 11. Hata hivyo, Simba yenye wastani wa magoli 12, inaendelea kuongoza
ligi kwa wastani wa goli moja zaidi ya Yanga yenye wastani wa magoli 11. Simba
imefunga magoli 20 na kufungwa 8 wakati Yanga imefunga magoli 21 na kufungwa
10.
Yanga ilianza kuhesabu goli la
kwanza katika dakika ya pili tu ya mchezo kupitia kwa beki wake wa kati Nadir
Haroub 'Cannavaro' aliyefunga kwa kichwa kufuatia mpira wa 'fri-kiki' uliopigwa
na kiungo Haruna Niyonzima.
Mshambuliaji Didier Kavumbagu aliifungia Yanga goli la
pili katika dakika ya 39 kufuatia krosi ya Hamis
Kiiza na Jerry Tegete akakamilisha ushindi wa kujiamini wa timu yake
wakati alipofunga goli la tatu katika dakika ya
79 kufuatia pasi ya Oscar
Joshua.
Ulikuwa ni
ushindi wa saba katika mechi 11 kwa Yanga na kuwasahaulisha mashabiki wao mwanzo
mbaya wa msimu uliowafanya wamfukuze kocha Mbelgiji Tom Saintfiet aliyedumu nao
kwa siku 80 tu huku akiwa ameshawapa ubingwa wa Afrika Mashariki na Kati (Kombe
la Kagame).
Yanga pia ilifurahia
kurejea kwa beki wake wa kati, Kelvin Yondani, aliyecheza kwa mara ya kwanza tangu aliponusurika kuumia vibaya
zaidi katika rafu mbaya ya "vunja mifupa" aliyochezewa na kiungo Haruna Moshi
'Boban' wa Simba katika mechi ya watani wa jadi
Oktoba 3. Aliingia katika dakika ya
46 akichukua nafasi ya beki veterani wa kulia,
Shadrack Nsajigwa.
Mambo hayakuwa mazuri kwa mabingwa Simba ambao
walitanguliwa kwa goli la dakika ya 33 kutoka kwa Mokili Lambo, aliyekuwa
ameingia uwanjani dakika 5 tu zilizopita kuchukua nafasi ya John Bosco
aliyepumzishwa katika dakika ya 28.
Simba walirejea kipindi cha pili wakiwa nyuma kwa
goli 1-0 kabla ya kiungo wao aliye katika kiwango cha juu tangu kuanza kwa msimu
huu Amri Kiemba kuwasazishia katika dakika ya 57 akimalizia kona iliyochongwa na
Emmanuel Okwi.
Ilikuwa ni sare ya 5
katika mechi 7 zilizopita za Simba baada ya kushinda zote nne za kwanza
mfululizo, wakati Polisi ilipata pointi yao ya tatu kutokana na sare tatu huku
ikiendelea kubaki mkiani mwa ligi ikiwa haina ushindi baada ya mechi 11.
Imefungwa mechi 8.
Sare nyingine
katika mechi za ugenini, ilionekana kumchanganya kocha wa Simba, Mserbia Milovan
Cirkovic ambaye alidai kwamba refa Jacob Ondongo kutoka Mara alichezesha vibaya
na kwamba alionekana kuipendelea timu mwenyeji.
Kocha msaidizi wa Polisi, Ally Jangalu aliwapongeza
wachezaji wake kwa kucheza vizuri akisema walikuwa na makosa katika upande wa
ufungaji lakini wamerekebisha kiwango tangu walipocheza dhidi ya Ruvu Shootings
ambapo walilala 2-1 kwenye Uwanja wa Mabatini mkoani Pwani.
Mgambo ambao waliwashikilia Simba katika sare ya
kustusha mkoani Tanga iliyochangia kusimamishwa kwa kiungo wa Wekundu, Haruna
Moshi 'Boban', walijikuta wakimaliza wakiwa 10 uwanjani baada ya beki wao Salum
Mlima kumchezea rafu beki wa Yanga, Mbuyu Twite katika dakika ya 85 na kutolewa
kwa kadi nyekundu na mwamuzi Martin Saanya wa Morogoro.
Coastal Union ya Tanga iliyo katika nafasi ya tatu
itajaribu kuitetea nafasi yake wakati itakapocheza ugenini dhidi ya Azam iliyo
katika nafasi ya nne kwenye Uwanja wa Azam Complex Chamazi
kesho.
Vikosi kwenye
Uwanja wa Taifa
vilikuwa:
Yanga:
Ally Mustapha 'Barthez', Shadrack Nsajigwa, Oscar Joshua, Nadir Haroub
'Cannavaro', Mbuyu Twite, Athumani Idd 'Chuji',
Simon Msuva, Frank Domayo/ Nurdin Bakari (dk.76), Didier Kavumbagu/ Jerry
Tegete (dk.68), Hamisi Kiiza na Haruna
Niyonzima.
Mgambo
JKT:
Godson Mmasa, Salum Mlima, Yasin Awadh, Salum Kipanga, Bakari Mtama, Ramadhan Malima, Chande Maguja, Issa Kanduli/ Nassor Gumbo (dk.59), Fully Maganga na Juma Mwinyimvua/ Omary Matwiko
(dk.76).
Vikosi kwenye
Uwanja wa Jamhuri vilikuwa:
Polisi Morogoro:
Aghaton Mkwando, Nahoda Bakari, John Bosco/ Mokili Lambo (dk.28),
Noel Msakwa, Hamis Mamiwa, Abdallah Mfuko, Bantu Admin, Maige Pascal, Ally Shomary, Malimi Busungu, Nicholaus
Kabipe.
Simba:Juma Kaseja, Nassor
Masoud 'Chollo', Amir Maftah, Pascal Ochieng,
Shomary
Kapombe, Jonas Mkude, Amri Kiemba, Mwinyi
Kazimoto, Felix Sunzu, Emmanuel Okwi na
Mrisho Ngassa.
No comments:
Post a Comment